Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesisitiza kuwa Yanga haijabebwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2019/20, bali nafasi hiyo wameitolea jasho.
Tangu Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilipotangaza kutoa nafasi nne kwa Tanzania kushiriki michuano yao, Yanga ikipata nafasi Ligi ya Mabingwa kuungana na Simba, mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakiwabeza watani wao hao wa jadi, kuwa wao ndio waliowabeba.
Hilo linatokana na ukweli kwamba kitendo cha Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ndio kilichochangia CAF kuiongezea Tanzania nafasi mbili zaidi kushiriki michuano yao, huku KMC ikiungana na Azam Kombe la Shirikisho.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Karia alisisitiza kuwa hakuna timu yoyote iliyobebwa kati ya Yanga na KMC, bali zimepata nafasi kulingana na kanuni.
“Kuhusu Simba kuwabeba Yanga kimataifa, hiyo sio ilivyo, Yanga wamejibeba wenyewe kwakufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho (Afrika) mara mbili na kufikisha pointi ambazo zimewapelekea kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao,” alisema Karia.
Kwa upande wa KMC, alisema nafasi hiyo ilibidi iwe ya timu ambayo imeshika nafasi ya tatu katika ligi ambayo ni Azam FC, lakini kwa kuwa Wanalambalamba hao ndio mabingwa wa msimu huu wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC2019), hivyo nafasi hiyo imechukuliwa na aliyemaliza ligi kwenye nafasi ya nne (KMC).
Karia alizitaka timu zote ambazo zimepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya kimataifa msimu ujao, kuitumia nafasi hiyo ipasavyo ili kuendelea kuipeperusha Bendera ya Tanzania kama ilivyofanya Simba.
No comments:
Post a Comment