WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa kesho Jumatatu atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano ya kitaifa ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania (Umisseta) yatakayofanyika mjini Mtwara.
Michezo hiyo itakayoshirikisha takribani washiriki 3,304 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara na miwili Zanzibar, itafanyika hadi Juni 21 na kufungwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof Joyce Ndalichako.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Idara ya Elimu (Tamisemi), Leonard Thadeo alisema jana kuwa kila kitu kimekamilika na tayari yeye na timu yake wako Mtwara kwa ajili ya michezo hiyo.
Alithibitisha kuwa Majaliwa ndiye atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa michezo hiyo mwaka huu, ambayo itashirikisha michezo ya soka, netiboli, riadha, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa mikono kwaya pamoja na ngoma.
Aidha, Thadeo alisema kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ndiye atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi (Umitashumta) utakaofanyika Juni 25 wakati wachezaji wataanza kuwasili siku mbili kabla.
Alisema kuwa michezo ya Umitashumta yenyewe itashirikisha mikoa 26 ya Tanzania Bara tu na inatarajia kufungwa Julai 3 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo.
Thadeo aliongeza kuwa lengo lao kubwa la kwanza ni kuwawezesha wanafunzi kucheza michezo, ambayo ni sehemu ya elimu na wale wanaohusika na kuendeleza vipaji wanatakiwa kuwaendeleza watoto hao.
No comments:
Post a Comment