By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi mwanzoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Profesa Kitila alitetea mfumo wa siasa za ushindani nchini huku akisema CCM ina faida ya kuwa madarakani, “nimeshiriki siasa za Tanzania tangu mwaka 1995, sijawahi kusikia vyama vya upinzani vikisema sasa ushindani uko sawa. Sijawahi kuona duniani kote chama cha upinzani kikatamba kuwa sasa uwanja wa ushindani uko vizuri. “Duniani kote, kuna kitu kinaitwa faida ya kuwa madarakani. Chama ambacho kiko madarakani kina ‘advantage’. Ukienda Marekani, Republican wana ‘advantage’. Ukienda Uingereza Conservative pamoja na yote wanayofanya wana ‘advantage’. Lakini vyama vilivyo upande wa pili vinapambana. Sasa hapa kwetu tuna vyama ambavyo vinafikiri vitapata chakula kwenye sahani. Nitajie duniani nchi gani unaweza kushinda ‘in silver plate’. Huwezi kushinda kwa huruma.”
Alivitaka vyama vya upinzani kuweka sera mezani na kuwa na uongozi bora, akitolea mfano wa siasa za Zambia na Malawi.
“Hapa kwetu kuna kulialia sana. Ni lini wamewahi kusema ‘playing ground iko level (uwanja wa mchezo upo sawa)? Lakini wameshinda ubunge, wameshinda kina Zitto (Kabwe), (Freeman) Mbowe wengi tu wameshinda ubunge Dar es Salaam hapa,” alisema Kitila.
Kuhusu muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Profesa Kitila alitetea uongozi wake kuteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.
“Nchi hii ni ya utawala wa sheria, nitajie nchi hapa duniani, viongozi wake hawateuliwi na Rais. Uingereza uchaguzi unasimamiwa na Serikali, tena wizara, siyo kwamba mwenyekiti anateuliwa na Serikali, lakini uchaguzi unasimamiwa na Serikali. Marekani ambao tunasema wana demokrasia iliyokomaa, uchaguzi unasimamiwa tena na Serikali ya jimbo linalohusika, tena wakati mwingine la upinzani.”
Sababu za kuhamia CCM
Akieleza sababu za kuhama upinzani, Profesa Kitila aliyewahi kuwa kada wa Chadema kabla ya kufukuzwa na wenzake Novemba 2013 na baadaye kuasisi ACT Wazalendo, alisema hilo ni jambo la kawaida duniani kote.
Profesa Kitila, ambaye baada ya kuteuliwa ukatibu mkuu wa wizara aliachana na ACT Wazalendo na kujiunga na CCM alisema amevutiwa na sera, itikadi na uongozi wa chama hicho tawala.
“Kwa sababu CCM ni chama cha ujamaa na kujitegemea, ndiyo itikadi yake na ndiyo maana nilipokwenda kule kwingine, nilitengeneza chama cha kijamaa, kwa sababuni ni kitu ninachokiamini. (CCM) kina mheshimiwa John Pombe Magufuli, kina Dk Bashiru Ally, ni watu ninaoendana nao, kihulka na kiitikadi, kwa hiyo nimefika nyumbani.”
Alisema sababu zake binafsi zilizomrudisha CCM ni kutotaka kutofautiana na Serikali ya chama anayotumikia. “Kuna dhana na uhalisia... natumikia Serikali ya CCM nakubaliana na yote wanayofanya halafu siko katika mfumo na sababu zilizofanya uhame hazipo, basi unaingia tu kwenye chama.”
Kuhusu msimamo wake wa awali alipokuwa upinzani, alisema sasa hawezi kulalamika kwa kuwa amepata fursa ya kujibu malalamiko, “nilikuwa na bahati wakati ule ya kulalamika, sasa nina fursa ya kutekeleza. Kwa hiyo mimi sasa niulizwe natekelezaje.”
Huku akitoa mifano ya wanasiasa duniani, Profesa Kitila alitetea uamuzi wake wa kuhama “Huyu (Donald) Trump, Rais wa Marekani alishahama vyama mara nne. Mwasisi wa kuhama vyama duniani ni Winston Churchill. Kwanza alikuwa Conservative akaenda Labor, akarudi Conservative akawa Waziri Mkuu (Uingereza). “Raila Odinga amehama mara ngapi? Hiki chama ni mara ya sita. Uhuru amehama vyama mara ngapi? Tatizo tuna ushamba wa kisiasa, ukisema mbunge amenunuliwa, kwani yeye ni bidhaa?
“Hilary Clinton alikuwa Republican, baadaye akaingia Democratic mpaka amegombea urais. Hapa Tanzania ukihama vyama ni taabu, ya nini? Watu wanaacha ndoa itakuwa chama cha siasa?” alihoji.
Alipoulizwa kama kuhama kwake kulitokana na kushawishiwa kimasilahi, Profesa Kitila alisema hakuwa na shida ya fedha kwani alishazipata alipofikia ngazi ya profesa wa chuo kikuu.
“Ukishakuwa Profesa, ulishamaliza njaa, unashughulikia mambo makubwa, kama ni watoto shule hufikirii, huwazi tena chakula, sifikirii nitavaa nini, sifikirii kujenga. Hayo mambo tulishayamaliza tulipokuwa profesa. Nilishamaliza siku nyingi na ukikuta profesa analia njaa, huyo kashachoka, lakini siyo profesa, ni yeye mwenyewe.”
Alisema uteuzi wake kuwa katibu mkuu ni nafasi kubwa ambayo wanataaluma wengi hawajaipata.
Akifafanua jinsi ilivyokuwa baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alisema ilimshtua, lakini kwa kuwa alikuwa mtumishi wa umma, alipandishwa cheo tu.
No comments:
Post a Comment