Mfanyabiashara maarufu ambaye ni Mwanchama wa Yanga Bilionea Rostam Aziz ameutaka uongozi wa timu hiyo kuachana na mfumo wa uendeshaji ambao ni tegemezi kwa mtu mmoja au wafadhili
Badala yake ijikite zaidi kwenye mfumo ambao utawawezesha wanachama wote kuwa wamiliki wa timu
Mwishoni mwa wiki iliyopita Rostam aliichangia Yanga Tsh Milioni 200 kwenye Harambee ya Kubwa Kuliko ambapo pia anatarajiwa kuonana na viongozi wa Yanga kwa ajili ya masuala mengine yanayohusiana na mchango wake wa klabu
"Kwa mtazamo wangu, Yanga haitakiwi kumilikiwa na mtu binafsi wala kutegemea ufadhili kwa sababu ni klabu yenye wanachama na mashabiki wengi," Rostam aliwaambia waandishi wa habari aliokutana nao nyumbani kwake Masaki leo
"Yanga inatakiwa kumilikiwa na wanachama wake wote. Kunapokuwa na ufadhili au umiliki wa mtu binafsi unawanyima au kuwabinya wale walio wengi hivyo naamini Yanga inatakiwa ibakie kwa wanachama"
"Ufadhili nao ni kama umiliki kwa sababu ufadhili ni mlango wa nyuma wa umiliki. Kwa sababu inawezekana kuna watu wanataka kuingia kwenye klabu, lakini wakahofia uwepo wako. Kwa hiyo huwezi kusema unapinga umiliki halafu wakati huohuo unasapoti ufadhili"
"Kuhusu udhamini sawa, binafsi niko tayari kuidhamini Yanga kupitia moja ya kampuni zangu. Lakini sikubaliani na umiliki wa mtu mmoja au ufadhili"
Katika Harambee ya uchangiaji wa Yanga, timu hiyo ilitumia kauli mbiu ya Timu ya Wananchi, Wawekezaji ni Wananchi ambayo inaashiria inakusudia kutumia mfumo tofauti wa uwekezaji
Wakati ikiwasilisha ripoti yake, Kamati ya Hamasa na Uchangishaji iliyokuwa chini ya Mh Anthony Mavunde, ilipendekeza kuendelezwa kwa mfumo wa uchangiaji ambapo iliutaka uongozi wa Yanga ukusanye takwimu sahihi za mashabiki na wanachama wake kisha utengeneze kanzidata ambayo itawasaidia kufahamu namna wadau hao wanaweza kushirikishwa katika kuiendesha timu
Aidha suala la kuandikisha Wanachama limetakiwa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa Yanga ambapo tayari uongozi wa Yanga unaandaa utaratibu wa kuandikisha wanachama kupitia simu za mkononi
Kwa hesabu ndogo tu , kama Yanga itakuwa na Wanachama Milioni moja ambao wanapaswa kulipa ada Tsh 12,000 kwa mwaka (Tsh 1000 kwa mwezi), itakuwa na uhakika wa kukusanya Bilioni moja kila mwezi fedha ambazo ni zaidi ya zinazohitajika kuiendesha timu hiyo kwa mwezi mmoja

No comments:
Post a Comment