KOCHA msaidizi wa zamani wa Simba, Masoud Djuma, anatajwa kutua katika kikosi cha KMC kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Djuma aliyetimuliwa na Simba mapema msimu uliomalizika hivi karibuni kwa madai ya kutoelewana na kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems, anakuja KMC kuchukua nafasi ya Ettiene Ndayiragije.
Ndayiragije aliyeiwezesha KMC kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao baada ya kushika nafasi ya nne Ligi Kuu Bara 2018/19, amekataa kuongeza mkataba mwingine, akiwa amemaliza wa awali wa mwaka mmoja.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu ya KMC, zimeeleza kuwa Djuma ana nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Mrundi Ndayiragije.
“Ijumaa iliyopita waliwasiliana na Djuma ambaye aliwataka wazungumze Jumatatu (leo) kwa kuwa alikuwa kwenye kozi ya ukocha nchini kwao Burundi na hakuwa katika muda mzuri.
“Mwakani KMC itashiriki mashindano ya kimataifa, wanahitaji benchi la ufundi bora ambalo litakuwa na mafanikio,” alisema mtoa habari huyo.
Chanzo hicho kinasema kuwa Djuma anatarajiwa kuongoza benchi la ufundi la timu hiyo, akisaidiwa na Seleman Matola ambaye msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Bara, alikuwa kocha msaidizi Lipuli.
BINGWA lilimtafuta Djuma kufahamu juu ya mpango huo wa KMC ambapo kocha huyo, alikiri kupokea simu kutoka Tanzania.
“Nimepokea simu moja ikiniuliza kama nina mpango wa kurudi huko, nyingine ikiniambia kutaka kufanya kazi na mimi, lakini nimewaomba wasubiri hadi Jumatatu (leo) au Jumanne (kesho) nitazungumza nao vizuri kwa kuwa nipo katika mafunzo, sitoweza kuzungumza nao vizuri,” alisema Djuma.
No comments:
Post a Comment