Akizindua ripoti ya taarifa ya Taasisi ya Wajibu jana jijini hapa, Profesa Assad alisema uwajibikaji ni neno pana ambalo maana yake ni kutoa taarifa kwa mtu ambaye anaihitaji.
Alisema katika nchi yoyote, kukusanya kodi ni jambo muhimu kwa maendeleo lakini lazima kodi hizo ziwe rafiki kwa wanaolipa.
Alisema kiwango cha kodi kikiwekwa kwa asilimia 0 ni tatizo na kikiwekwa kwa asilimia 100 ni shida pia.
Alitaja kero zinazowapata baadhi ya wafanyabiashara kuwa ni kutokupewa kiwango stahiki cha kodi na kusababisha kukimbia na kufungiwa licha ya kuwa wengine wanaumizwa na utaratibu wa kutojua umuhimu wa ulipaji kodi.
“Na mimi naamini katika nchi hii ili kuongeza uwajibikaji tunahitaji vitu viwili; taasisi za umma ambazo ni za usimamizi na uchunguzi na hizi zinahitaji kuwa imara zenye misingi mizuri lakini pia ziwe na watu wenye uwezo, na eneo la pili kama taasisi za kijamii nazo zikiwa nzuri, zenye watu wenye uwezo kufanya kazi zake, taifa litakwenda mbele,” alisema Profesa.
Alisema ni muhimu taasisi za kijamii zipige kelele pale ambako zile za Serikali haziwezi ili mambo yaende vizuri zaidi.
Mkurugenzi wa taasisi ya Wajibu, Ludovick Utouh alisema ripoti hiyo ambayo ni ya tatu, hutoa taarifa za uwajibikaji zinazotokana na ripoti za CAG zinazowasilishwa bungeni.
Utouh alisema ripoti za CAG ni kubwa, zaidi ya vitabu vitatu hadi vinne yenye kurasa 300 au 400 na kutengeneza kurasa 20 au 22.
Alisema ukaguzi wa CAG hufanywa kwa nia njema kwa kutumia Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 ambayo inampa mamlaka kisheria ya kutoa mapendekezo ya kuboresha makusanyo ya rasilimali za Taifa na matumizi yake.
Hata hivyo, alisema ni jukumu la Watanzania wote kutafakari ni kwa nini mwisho wa mwaka makusanyo hayaendani na bajeti halisi iliyopitishwa hivyo watambue sababu za kwa nini Serikali isikusanye zaidi.
“Mapato yatokanayo na kodi na mapato ambayo hayatokani na kodi, ni jukumu la Watanzania wote kwa sababu Serikali inahitaji pesa nyingi kwa ajili ya maendeleo, lazima tujiulize kwa pamoja tunafanyaje kuboresha,” alisema.
Alisema miradi mikubwa ya Serikali ni ya fedha nyingi ambazo zinatoka kwa Watanzania mmojammoja ama kupitia kodi au mapato mengine ambayo hayahusu kodi.
No comments:
Post a Comment