Zaidi ya kampuni kubwa 30 za uwekezaji katika sekta ya mafuta zimeiomba serikali kuharakisha mradi wa kuchakata gesi asilia mkoani Mtwara.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam wakati Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) ilipokutana na wafanyabiashara hao ikiwa ni mwendelezo wa kukaa na taasisi mbalimbali kujadiliana na kubaini changamoto za wafanyabiashara ambazo huwasilishwa serikalini ili zitatuliwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, akizungumza kwenye mkutano huo, alisema moja ya changamoto ambazo zimeonekana ni ya mradi wa kuchakata gesi asilia, kutokuwa na dalili za kuendelea.
“Tumekutana na sekta ya mafuta na gesi ili kujadili changamoto zao na moja ya changamoto waliyotueleza ni mradi wa kuchakata gesi Mtwara, hivyo tunaomba serikali iuharakishe," alisema.
Pia alitaja changamoto nyingine iliyoainishwa kwenye mkutano huo kuwa ni mikataba ya makubaliano ya uzalishaji na mauzo ya gesi na mafuta (PSA) ambayo serikali iliichukua ili kuiangalia upya ambayo alisema imechukua muda mrefu.
“Wametueleza kuwa mikataba hii ilichukuliwa na serikali na wao wanalalamika kuwa suala hilo limechukua muda mrefu, hivyo wanaomba kuharakishwa,” alisema.
Simbeye alisema wiki tatu zilizopita TPSF ilikutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye aliahidi mpaka mwishoni mwa mwezi huu, kazi ya kuipitia mikataba hiyo itakuwa imekamilika.
No comments:
Post a Comment