MAAM-BUKIZI sugu ya njia ya mkojo (Chronic Urinary Tract Infections – U.T.I) ni maambukizi kwenye njia ya mkojo ambayo hayatibiki kwa urahisi au yanajirudia mara kwa mara baada ya tiba. Maambukizi haya yanaweza kuendelea kuathiri njia ya mkojo hata baada ya kupata matibabu sahihi au yanaweza kujirudia muda mfupi baada ya matibabu. Njia ya mkojo huunda mfumo wa mkojo ukiwa na ogani mbalimbali kama figo, ureta (mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye figo kwenda kwenye kibofu cha mkojo), kibofu cha mkojo na urethra (mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo kutoa nje).
Maambukizi kwenye njia ya mkojo yanaweza kutokea sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo. Ikiwa maambukizi yataathiri kibofu cha mkojo peke yake ni rahisi hali hii kutibika, isipokuwa maambukizi yakisambaa mpaka kwenye figo, unaweza kuumwa zaidi na pengine kulazwa hospitali.
Ingawa maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kumpata yeyote, wakati wowote bila kujali jinsia na umri, maambukizi haya hutokea sana kwa jinsia ya kike. Tafiti ya National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases (NIDDK) inakadiria kila wanawake watano kuna mmoja anasumbuliwa na maambukizi ya njia ya mkojo yanayojirudia mara kwa mara.
Yafuatayo huongeza hatari ya maambukizi sugu ya njia ya mkojo. Maambukizi sugu ya njia ya mkojo huwapata sana jinsia ya kike kutokana na maumbile yao.
Kwanza, urethra ipo karibu sana na njia ya haja kubwa au puru (rectum) kwa wanawake kitu kinachorahisisha bakteria kutoka kwenye puru kuingia kwenye urethra hasa ukichamba/ kutawadha kwa kurudisha mkono kutoka nyuma kwenda mbele. Hii ni moja ya sababu kubwa ya watoto wadogo wa kike kupata maambukizi ya njia ya mkojo kwa kuwa bado hawajajifunza jinsi ya kuchamba vizuri.
Pili, urethra ya mwanamke ni fupi zaidi ikilinganishwa na ya mwanaume. Hii ina maana bakteria wana umbali mfupi zaidi wa kusafiri kufika kwenye kibofu cha mkojo ambapo wanaweza kuzaliana na kuongezeka kiurahisi na kusababisha maambukizi.
Kuna aina ya maisha ambayo yanaweza kukufanya uwe kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi sugu ya njia ya mkojo kwa urahisi. Kwa mfano kutumia diaphragm (mpira laini maalum unaowekwa ukeni wenye kizibo cha kuzuia mbegu za mwanaume kupenya ili kukutana na yai la mwanamke) inaweza kusukuma juu urethra na kufanya iwe vigumu kutoa mkojo wote baada ya kukojoa. Mkojo unaobaki kwenye kibofu huongeza uwezekano wa bakteria kuzaliana na kusababisha maambukizi.
Mfano mwingine ni pale mwanamke anapobadili muundo wa kinga ndani ya uke wake kwa kutumia vitu vyenye kemikali kuosha uke wake, zinazoua bacteria walinzi wa kwenye uke, kama sabuni, marashi au viua shahawa (spermicides). Pia, kunywa dawa za kuua bakteria mwilini huweza kuua bakteria walinzi kwenye uke. Hii inaweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi sugu ya njia ya mkojo.
Kukoma hedhi pia husababisha mabadiliko ya homoni, ambayo mwisho husababisha kubadilika kwa hali ya bakteria walinzi ndani ya uke hivyo kufanya wafe kwa wingi na uke kukosa ulinzi na kufanya iwe rahisi kupata maambukizi ya njia ya mkojo mara kwa mara. Ili kujua dalili, madhara na tiba ya tatizo hili, fuatilia hapahapa
No comments:
Post a Comment