Wakizungumza na Mwananchi, viongozi wa vyama hivyo wameanika umuhimu wa kushiriki uandikishwaji huo kwa maana ya kufikisha elimu ya uraia kwa wananchi, huku viongozi wengine wa upinzani wakilalamikia vikwazo vya kisheria na mazingira ya kufanya siasa nchini.
Jana bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde alisema kwa mujibu wa kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Uchaguzi sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) iko katika hatua za mwisho za kufanya maandalizi ya uboreshaji wa daftari kwa ajili ya majaribio katika baadhi ya mikoa.
Mavunde alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza mchakato wa kuboresha daftari hilo.
Awali, akizungumza na Mwananchi, mkurugenzi wa Nec, Dk Athuman Kihamia alisema taarifa za kuanza kwa uboreshaji wa daftari hilo zitatolewa baadaye.
Akizungumzia wapigakura wapya watarajiwa, makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema licha ya kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa chama hicho kinazo mbinu za kuwafikia wapigakura hao.
“Tunazo strategies zetu ambazo nisingependa kuziweka wazi kwa sababu tumezuiliwa kufanya mikutano wakati CCM inafanya waziwazi, elimu ya uraia haiwezi kuwafikia bila ushiriki wa vyama vya upinzani kupitia mikutano ya kisiasa,” alisema.
Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Ngemela Lubinga alisema kundi hilo la wapigakura watarajiwa litakuwa sehemu ya makundi ambayo hufikiwa na chama hicho wakati wa ushawishi wa kutambua umuhimu wa kupiga kura.
“CCM imekuwa ikishawishi wanachama wake na umma kwa ujumla katika kutambua haki zao za kupiga kura, CCM tumejipanga siku zote (kuwafikia),” alisema Lubinga.
Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe alisema mbinu za kudhoofisha upinzani nchini ni changamoto ya kulifikia kundi hilo la wapigakura.
Rungwe alisema bila ushiriki wa vyama hivyo, idadi ya wapiga kura itaendelea kupungua wakati wa chaguzi. “Tumepigwa breki ya kufanya siasa na refa yupo upande wao, tutafanyaje? Matokeo yake idadi ya wapigakura inapungua kwa sababu hawaoni umuhimu tena,” alisema.
Upinzani na mikutano
Katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabi alisema vyama vya upinzani vinakubalika zaidi kwa vijana na kwamba wao wapinzani wana nafasi kubwa ya kuwahamasisha kutambua umuhimu wa haki hiyo kikatiba, lakini wanazuiwa kufanya mikutano.
Katibu mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema pamoja na zuio la uhuru wa mikutano ya kisiasa, maboresho ya Sheria ya Vyama vya Siasa iliyopitishwa na Bunge siku chache zilizopita inaweka vikwazo kwa vyama kuhusu mikutano ya uelimishaji wananchi na haoni usawa wa vyama kuwafikia wapigakura hao wapya.
Mwaka 2015, Nec iliboresha daftari hilo kwa kutumia mfumo wa teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR) na kusajili wapigakura 22,750,789.
Kwa ongezeko la wapigakura wapya milioni nne ina maana kwamba ifikapo 2020 wapigakura watafikia takriban milioni 27.
Hata hivyo, wakati Nec ikisubiriwa kutangaza tarehe ya kuanza uboreshaji wa daftari, uchambuzi wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kupitia MwananchiData umebaini vijana zaidi ya 5,700,000 wanasubiri kupata haki hiyo.
Vijana hao ni wale ambao wakati wa Uchaguzi Mkuu 2015 walikuwa na umri wa kati ya miaka 13 hadi miaka 17 ambao mwakani watakuwa na miaka 18 na 22, kwa mujibu wa ripoti ya makisio ya idadi ya watu nchini iliyotolewa Februari mwaka jana na NBS.
No comments:
Post a Comment