Mahakama Kuu imeyakataa maombi ya Serikali ya kupewa muda zaidi ya ule unaoelekezwa kisheria kuwasilisha utetezi wake katika kesi ya kikatiba inayomkabili Spika Job Ndugai, badala yake imetoa siku 14 kuwasilisha utetezi huo kama sheria inavyoelekeza.
Pia, Mahakama imepanga kusikiliza rasmi kesi hiyo Februari 15, ambako mlalamikaji Zitto Kabwe atatoa hoja zake na wadaiwa ambao ni Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), watatoa utetezi wao kwa kujibu hoja hizo na kusubiri uamuzi wa Mahakama. Kesi hiyo ya kikatiba namba 01 ya 2019 imefunguliwa na Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini, dhidi ya Spika Ndugai na AG, ikihusu kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Zitto ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo anaiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaotuhumiwa kudharau Bunge. Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watu - Firmin Matogolo (kiongozi wa jopo), Benhajj Masoud na Elinaza Luvanda ilitajwa jana mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na wakili wa Serikali Mkuu, Alesia Mbuya akaomba muda zaidi wa kuwasilisha utetezi.
Mbuya aliyeongoza jopo la mawakili watatu wa Serikali waliowawakilisha wadaiwa, aliieleza Mahakama kuwa walipata wito wa kufika mahakamani hapo juzi mchana na akaomba wapewe muda zaidi ya ule unaoelekezwa kisheria wa siku 14 kuwasilisha utetezi.
“Hivyo tunaomba muda zaidi wa kuwasilisha utetezi, zaidi ya siku 21 yaani mpaka Februari 28 (mwaka huu). Sababu ni kwamba kwa sasa vikao vya Bunge vinaendelea na mteja wetu muhimu ni Spika, hivyo tunahitaji kupata muda wa kutosha kujadiliana naye,” alidai Mbuya. Hata hivyo, maombi na hoja hiyo vilipingwa na wakili wa Zitto, Fatma Karume aliyedai kuwa sheria inapaswa kuzingatiwa kwa watu wote na kwamba Spika ana wasaidizi wengine akiwamo naibu wake ambaye anaweza kutekeleza majukumu hayo wakati yeye hayupo.
Alidai kwamba wabunge na hasa wa upinzani wanaposhtakiwa wamekuwa hawapewi nafasi ya kuendelea na majukumu yao ya kibunge, badala yake wanalazimika kufika mahakamani kwanza kuendelea na kesi bila kujali uwakilishi wa wapiga kura wao.
Akitoa uamuzi, Jaji Matogolo alitupilia mbali maombi na hoja za Serikali kuongezewa muda na kuamuru wadaiwa kuwasilisha utetezi ndani ya siku 14 kama sheria inavyoelekeza na akapanga usikilizwaji wa kesi hiyo Februari 15.
Zitto alifungua kesi hiyo baada ya Spika Ndugai kupitia vyombo vya habari na baadaye kumwandikia barua CAG kumtaka afike mbele ya Kamati ya Bunge ya Kinga, Haki na Madaraka kuhojiwa kutokana na madai kuwa alitoa kauli akiwa nchini Marekani kuwa Bunge ni dhaifu.
Profesa Assad alidaiwa kutoa kauli hiyo wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa kulingana na namna ambavyo taarifa zake za ukaguzi zinavyofanyiwa kazi. Hivyo Zitto anaiomba Mahakama itoe tamko na kuamuru kuwa Spika alishindwa kuzingatia wajibu wake wa kufuata Katiba katika amri yake ya kumtaka CAG kufika mbele ya kamati Januari 21. Pia anataka Mahakama itamke na kuamuru kwamba amri hiyo ni kinyume cha Katiba na inakinzana na masharti ya ibara za 26 (1), 18(a) (b) na (d) za Katiba ya Tanzania na kwamba wito huo ni batili.
Vievile, Zitto anaiomba Mahakama hiyo itoe zuio la kudumu kumzuia Spika, watumishi na au wakala wake kutokuchukua hatua yoyote ikiwamo kuamuru au kuelekeza mtu yeyote kumkamata na au kumchukua CAG kwenda Dodoma kuhojiwa na kamati kuhusu kauli yake hiyo.
No comments:
Post a Comment