Januari 23, mwaka huu Raia John Magufuli alikutana na viongozi wa dini. Alitaka wamshauri na wengi walionekana wakimsifia badala ya kumpa ushauri.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Lyimo aliwakonga wengi wenye misimamo inayokinzana, alipomuomba Rais Magufuli kuwaachia uhuru wananchi wazungumze inapowezekana kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.
Lyimo alisema Watanzania wengi wanahofu hata kama haambiwi na watendaji wake, ila wengi hawathubutu kuzungumza licha ya kuwa anafanya mambo mengi mazuri.
Huyo ndiye alitokeza kama nyota wa mazungumzo. Alisifiwa kweli. Viongozi wengine walipokea kejeli mbalimbali. Wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Godbless Lema (Arusha Mjini), waliongoza mashambulizi kupitia ujumbe wa Twitter.
Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe aliamua kuwarudi Chadema, akawataka wawaombe radhi viongozi wa dini, akawaonya kwamba wasipofanya hivyo watatumbukia kwenye shimo ambalo hawatatoka.
Lema na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa, wamesharudisha majibu kwa Kakobe. Lema alisema kabla ya viongozi wa dini kuhitaji heshima, lazima wao waanze kumheshimu Mungu. Msigwa amesema Kakobe ndiye ametumbukia shimoni.
Msigwa amekumbusha kuwa Kakobe alipata kusema Serikali haitapitisha umeme mkubwa mbele ya Kanisa lake lakini ulipita, vilevile mwaka 2000 alizunguka na Augustino Mrema Tanzania nzima alipogombea urais kwa tiketi ya TLP, akidai alioteshwa na Mungu kuwa angeshinda urais. Msigwa anataka Kakobe asiaminike.
Wakati Msigwa na wengine wa Chadema wakitaka Kakobe asiaminike, sina uhakika kama wamesahau kuwa alikuwapo kwenye Mkutano Mkuu wa Chadema mwaka 2015, uliompitisha Edward Lowassa kuwa mgombea urais wa chama hicho.
Sina uhakika kama hao wanaomsema wamesahau kuwa Kakobe alikuwepo katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, Chadema walipozindua kampeni zao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2015. Na walimpa kipaza sauti na mimbari akahutubia. Mwaka 2015 aliaminika, 2019 asiaminike.
Kakobe kasema hajawahi kukutana na Lowassa na kuzungumza. Ni katika kuhakikisha anawakana Chadema jumla. Sidhani kama naye amesahau hotuba zake kwenye Mkutano Mkuu Chadema na uzinduzi wa kampeni mwaka 2015 za kumnadi Lowassa.
Chanzo cha mvutano wa Kakobe na Chadema ni siasa za kushikana uchawi. Wanasiasa walianza kurusha lawama kwa viongozi wa dini kwamba hawakusema walichopaswa kusema mbele ya Rais.
Walitaka kilichosemwa na Mchungaji Lyimo kuhusu uhuru na demokrasia na kila mmoja angezungumza hivyohivyo.
Baada ya kuona viongozi wa dini wakimsifia zaidi Rais, wanasiasa walitakiwa kugundua kwamba bado wana kazi kubwa ya kuuelimisha umma ili wanayoyaona hayapo sawa, yawe kwa kila Mtanzania. Wajibu wa mwanasiasa ni kufanya siasa. Viongozi wa dini jukumu lao ni kuhubiri neno la Mungu.
Ilitakiwa baada ya mkutano wa Rais Magufuli na viongozi wa dini, wanasiasa wa upinzani nao waombe kukutana nao kwa mazungumzo ili wawaelimishe masuala ya msingi wanayoona yanatakiwa kusemwa na kila mtu, hasa yale ya kikatiba, kama uhuru binafsi na demokrasia.
Kukimbilia kuwashambulia ni dalili ya ghadhabu Na ghadhabu ni ishara ya kushindwa. Wanatakiwa kuondoa jazba pale yanaposemwa wasiyopenda au wasiyempenda anaposifiwa. Hayo ndiyo demokrasia wanayoipigania.
Demokrasia siyo kutendewa haki wewe tu, bali na haki za wengine vema kuziheshimu. Kama viongozi wa dini wanaona Rais Magufuli anafanya vizuri, acha wamsifie. Ni wajibu wao kuyaonesha maeneo ambayo watu wanatakiwa kuyatazama ili wasimsifu Magufuli.
Rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru, Nelson Mandela aliposhutumiwa na mataifa ya Magharibi kwa urafiki wake na viongozi wa Cuba na Libya, aliwajibu, “Kuna watu wanataka maadui zao wawe maadui zetu.”
No comments:
Post a Comment