Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaagiza Mawaziri wa Afya na TAMISEMI kukutana ili kupitia upya muundo wa Kada ya Ustawi wa Jamii Nchini ili uendane na mahitaji ya utoaji huduma za Ustawi wa Jamii Nchini na kuitaka Wizara husika kuhakikisha inakamilika kazi hiyo mapema.
Amesisitiza kuwa Serikali inataka kila Sekta kuchangia katika Maendeleo ya Nchi hivyo kuwataka viongozi wa Wizara zote mbili kuharakisha mapendekezo ya muundo huo ili kuharakisha kasi ya maendeleo na kuwataka kumpatia majibu ya kasi hiyo haraka iwezekanavyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hayo wakati wa kufungua mkutano wa mwaka wa kiutendaji wa wataalamu wa ustawi wa Jamii kutoka Sekretarieti za mkoa na Mamlaka za Mitaa leo mjini Dodoma.
Aidha Waziri Mkuu amezitaka Sekretarieti za Mkoa na Mamlaka za Mitaa kote nchini kuhakikisha wataalamu wa Kada ya Ustawi wa Jamii wanaanza kuingia katika vikao vya managementi ili masuala ya Ustawi wa Jamii yapewa kipaumbele lakini pia kuitaka TAMISEMI kuhakikisha kazi zao zinaingizwa katika mipango ya bajeti.
Aidha Waziri Mkuu amewataka Maafisa hao kutumia vyema Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010 pamoja na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu ya Mwaka 2008 ili kuwarejeshea wananchi utu wao pale ambapo kuna dalili za kupoteza haki zao kwa kukosa huduma stahiki.
Aidha amezitaka Halmashauri zote chini kuendelea kuhainisha mahitaji sambamba na kuomba vibali vya ajira za Watumishi wa Kada za Ustawi wa Jamii ili kukabiliana na upungufu wa watumishi wa kada hiyo katika ngazi za Wilaya na Mikoa baada ya Maafisa hao kumuomba kufanya hivyo katika maombi yao.
Wakati huo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika hotuba yake fupi kwa mgeni rasmi amesema Wizara yake iko katika hatua nzuri ya kuufanyia marekebisho muundo wa Maafisa wa Ustawi wa Jamii Nchini lakini pia kutayarisha Sheria ya Ustawi wa Jamii pamoja na kuundwa kwa baraza la taaluma la wataalamu wa Ustawi wa Jamii Nchini.
Aidha amemwabia Waziri Mkuu Majaliwa kuwa Wizara yake ndiyo yenye jukumu la kutoa huduma kwa makundi yenye mahitaji maalum ya wazee, watoto na watu wenye ulemavu hivyo kuwakumbusha maafisa ustawi wa Jamii kuwa wanakazi kubwa ya kuhakikisha wanatoa huduma stahiki kwa walengwa.
Aidha Dkt. Ndugulile alimwambia Waziri Mkuu kuwa Serikali kwa sasa inatoa mikopo kwa walemavu kwa kutumia asilimia 2 ya mapato ya ndani ya Halmashauri tofauti na awali ambapo mikopo hiyo ikuwa kwa akina mama na vijana pekee ambapo fedha hiyo ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri.
Dkt Ndugulile pia alisema kumekuwepo ongezeko la vituo vya kulelea watoto laki ni kuna baadhi ya watumishi wa vituo hivyo ambao sio waaminifu kwani wale wasio waaminifu wanatumia watoto hao kwa kuwatumikisha kingono, kuwafanyisha kazi za utumwa, lakini pia kuwageuza ombaomba hivyo kuwataka maafisa ustawi wa jamii kuchunguza na kufunga vituo vyote vinavyofanya kinyume cha sheria.
Kwa mantiki amewaagiza Maafisa ustawi wa Jamii kuhakikisha wanafuatilia utendaji wa vituo vya kulele watoto wanasajiliwa na mamlaka husika lakini pia vianatoa taarifa ya robo mwaka, nusu mwaka na mwaka kwa maafisa ustawi wa Jamii wa Wilaya na Halmashauri zote Nchini.
Mkutano wa Mkuu wa mwaka wa kiutendaji wa wataalamu wa ustawi wa Jamii kutoka Sekretarieti za mkoa na Mamlaka za Mitaa wanakutana Dodoma kwa Siku tatu kwa lengo la kukumbushana kuhusu utendaji kazi wao lakinni pia maadili yao kazi na namna bora kudumisha kazi za ustawi wa Jamii Nchini.
No comments:
Post a Comment