Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekanusha habari inayosambaa katika mitandao ya kijamii ikidai kuwa TRA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Benki Kuu yaTanzania (BoT), inatangaza nafasi za kazi 500 za uelimishaji wa namna ya uchangiaji kodi pamoja na ukusanyaji waKodi ya Majengo vijijini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, wananchi wameombwa kuipuuza habari hiyo.
“TRA inakanusha taarifa hiyo na inauomba umma kuipuuza kwa sababu haina ukweli wowote”. Ilifafanua taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, hata mawasiliano yaliyopo kwenye habari hiyo potofu siyo mawasiliano rasmi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania hivyo wananchi wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka kutapeliwa.
Kumekuwepo na taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari "Mamlaka ya Mapato Tanzania(Tanzania Revenue Authority) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu (BOT)", ikieleza kuhusu TRA kutangaza ajira 500 ambayo imesababisha mamlaka hiyo kukanusha na kuwatahadharisha wananchi kuhusu taarifa hiyo potofu.
TRA imewaomba wananchi kupiga simu bure Kituo cha Huduma kwa Wateja kupitia namba 0800 750 075 au 0800 780 078 au kutuma barua pepe: huduma@tra.go.tz, au kutembelea tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania: www.tra.go.tz. Pia, wanaweza kutuma ujumbe kwa njia ya WhatsApp kwenda namba 0744-233-333 ili kupata ufafanuzi wa masuala yoyote yanayoihusu mamlaka hiyo.
No comments:
Post a Comment