Kwa mara nyingine tena Simba imedhihirisha kuwa ni wababe wa soka la Tanzania baada ya kuifumua Azam Fc mabao 4-2 katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa uwanja wa Uhuru
Shabani Idd Chilunda alitangulia kuifungia Azam Fc bao la kuongoza kwenye dakika ya 14, hata hivyo Azam Fc ni kama walichokoa nyuki kwenye mzinga kwani Simba ilisawazisha bao hilo baada ya dakika tatu tu kupitia kwa kiungo fundi wa mpira Sharaff Elden Shiboub aliyemalizia kwa kichwa shuti la Hassani Dilunga lililopanguliwa na mlinda lango wa Azam Fc, Razak Abarola
Ulikuwa ni usiku wa kuandika historia kwa Shiboub ambaye aliifungia Simba bao la pili kwenye dakika ya 23 akiunganisha vyema kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Mohammed Hussein
Mpaka mapumziko Simba ilikuwa mbele kwa mabao 2-1
Clatous Chama aliyeingia kuchukua nafasi ya nahodha John Bocco, aliipatia Simba bao la tatu kwenye dakika ya 57
Azam Fc ikarejea mchezoni kwenye dakika ya 78 kupitia bao la Frank Domayo
Hata hivyo kiungo Francis Kahata alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Azam Fc akifunga bao la nne kwenye dakika ya 85
Simba imeweka rekodi ya kutwaa Ngao ya Jamii kwa misimu mitatu mfululizo ikiwa sasa imetwa jumla ya Ngao tano tangu kuanzishwa kwa mfumo huo
No comments:
Post a Comment