Katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri, kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems, ameonyesha hataki utani baada ya kuwataka wachezaji wake kuwa makini na wasipoteze mipira kirahisi. Simba wanajiandaa na mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji Jumapili Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa mjini Beira nchini Msumbiji, Simba walitoka sare ya kutofungana na wenyeji wao UD Songo.
Aussems alionyesha hayo katika mazoezi ya jana yaliyofanyika viwanja vya Gymkhana jijini hapa kujiandaa na mchezo huo wa marudiano. Wachezaji hao walianza kufanya mazoezi ya viungo na baada ya hapo walifanya mazoezi ya kumiliki mpira kwa muda mrefu huku wakirudia zoezi hilo mara kwa mara. Baada ya kumaliza zoezi hilo, Mbelgiji huyo alianza kuwafanyisha mazoezi ya kufunga ambako mabeki wa pembeni walikuwa wakipiga krosi huku washambuliaji wakimalizia kufunga mbele ya mabeki wa kati ambao nao walitakiwa kuzuia. Katika zoezi hilo, kocha Aussems alionekana kuwa mbogo zaidi pale mchezaji alipokuwa akipoteza mpira kirahisi au kutokuwa makini.
Kikosi cha kwanza ambacho kocha huyo alikipanga walikuwa wachezaji, Beno Kakolanya, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Gadiel Michael, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Sharaf Eldin Shiboub, Francis Kahata, Rashid Juma, Deo Kanda, Tairone da Sliva na Clatous Chama. Aishi Manula, Kennedy Juma, Gerson Fraga Viera, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Miraji Athumani, Haruna Shamte, Said Ndemla na Yussuph Mlipili walikuwa katika kikosi cha pili.
Kwa mujibu wa Mtanzania digital, Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Aussems alisema anaendelea kukinoa kikosi chake huku akiyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza mechi za nyuma. “Wachezaji wote wanaonekana kupambana kwani nahitaji umakini zaidi kuhakikisha hatufanyi makosa kwenye mchezo wetu wa marudiano ukizingatia ndio utaamua hatima yetu ya kusonga hatua inayofauta,” alisema. Aussems alisema kwa kipindi hiki kilichosalia, anaamini watakaa sawa na kufuata kile ambacho wanakihitaji kabla ya kushuka dimbani Jumapili.
No comments:
Post a Comment