Viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja wametakiwa kuwasaidia viongozi waliochaguliwa kuteleleza ilani na ahadi walizozitoa wakati wa uchaguzi uliopita badala ya kukumbatia wagombea wa uchaguzi ujao.
Akifungua mafunzo ya siku moja yaliyoshirikisha viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM mkoani humo, Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Eddington Kisasi alieleza kuwa kufanya hivyo kunapelekea viongozi waliopo madarakani kushindwa kusimamia ahadi zao.
Alisema wapo baadhi ya viongozi wa chama lkatika ngazi mbali mbali wameanza kuwakumbatia wanachama ‘wanaojipitishapitisha’ kwa lengo la kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao watambue kuwa kufanya hivyo wakati huu ni kukiuka kanuni za uchaguzi za chama hicho.
Mafunzo hayo yaliyolenga kuhamasisha ujasiriamali na mikopo kwa wanawake na uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliandaliwa kwa pamoja kati ya mbunge wa viti maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Angelina Adam Malembeka na UWT Mkoa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi iliyoagiza kuinuliwa kwa hali za kiuchumi za wanawake katika ngazi zote.
Alisema kanuni za uchaguzi za CCM zinakataza mtu kufanya kampeni kabla ya wakati hivyo viongozi wanaoandaa wagombea na kupanga nao mikakati wanapaswa kujua kuwa wanachochea vurugu ambazo zinakwaza kasi ya utekelezaji wa ilani na kuchelewesha upatikanaji wa maendeleo ya jamii.
“Chama kiliweka muongozo na ndio maana Mwenyekiti wetu (Dk. John Magufuli) alikataza Mambo ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ili tupate kuteleleza ahadi tulizoweka kwa wananchi wetu na nyinyi no mashahidi kwamba kabla ya 2020 tumeshatekeleza ilani kwa zaidi ya asilimia 90 Tanzania bara na Zanzibar”, alieleza Kisasi.
Aidha aliwataka viongozi hao kuwa mabalozi wazuri na kuisambaza elimu waliyopatiwa kwa wanachama wenzao kwani yana umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii na siasa za Tanzania.
“Tuliahidi kuinua uchumi wa wanawake katika ilani ya uchaguzi kupitia njia mbali mbali zikiwemo za ujasiriamali na uanzishwaji wa viwanda hivyo mafunzo haya yana mchango mkubwa katika kuendeleza vikundi vya kiuchumi tulivyonavyo katika shehia, wadi, wilaya na mikoa yetu”, alisema Makamu huyo wa Mwenyekiti.
Aidha aliwataka wajasiriamali nchini kutumia fursa ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki iliyoanza Juni mosi mwaka huu Tanzania bara, kutengeneza mifuko mbadala ya kubebea bidhaa na kuipeleka huko ili kujiendeleza kiuchumi.
No comments:
Post a Comment