Vikosi vya Usalama nchini Sudan vimerusha mabomu ya machozi na kutumia risasi halisi kuwatawanya waandamanaji mjini Khartoum. Watu wanne wameripotiwa kuuawa katika siku ya kwanza ya mgomo wa kitaifa, kwa mujibu wa madaktari wanaoegemea upande wa upinzani. Wanaharakati wameitisha maandamano ya kupinga utawala huo kuanzia Jumapili, siku kadhaa baada ya msako wa kijeshi uliyosababisha vifo vya makumi ya watu katika mji mkuu wa Khartoum.
Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Wafanyikazi kadhaa wa benki, uwanja wa ndege na pamoja na wa shirika la umeme nchini Sudan wamekamatwa kabla ya mgomo wa kitaifa wa kupinga utawala wa kijeshi, linadai kundi kuu la waandamanaji. Chama cha wataalamu wa Sudan kinasema kuwa wafanyikazi pia wanatishiwa na mamlaka nchini.
Baraza la jeshi linalotawala nchi hiyo (TMC) halijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo.
Jeshi lilichukua uongozi baada ya kumg’oa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashir mwezi Aprili, na kuahidi kurejesha utawala wa kiraia baada ya kipindi cha mpito.
Lakini wanaharakati wa kupigania demokrasia wanasema kuwa baraza la jeshi haliwezi kuaminiwa baada kuzuka kwa ghasia ambapo wafuasi wengi wa Upinzani waliuawa mjini Khartoum – na wamekata kufanya mazungumzo ya amani na viongozi wa baraza hilo.
Huku hayo yakijiri vikosi vya usalama nchini Sudan vimewakamata viongozi watatu wa upinzani baada ya kukutana na waziri mkuu wa Ethiopia mjini Khartoum ili kusaidia katika mazungumzo ya amani.
Hali ikoje mjini Khartoum?
Baadhi ya maofisi na biashara zimefungwa na idadi ya magari ni chache barabarani, anasema mwandishi wa BBC Catherine Byaruhanga ambaye anafuatilia matukio nchini Sudan.
Kumeripotiwa milio ya risasi huku maafisa wa usalama wakiendelea kushika doria katika baadhi ya sehemu za mji waKhartoum.
Viongozi wa maandamano wametoa wito kwa watu kusalia majumbani mwao na kususia kazi kama sehemu ya kupinga utawala uliyopo madarakani.
Wanasema maandamano hayawezi tena kufanyika kutokana na msako mkali unaoendeshwa na vikosi vya usalama.
“Viguvugu la kususia kazi linaanza Jumapili na litaendelea hadi pale utawala wa kiraia utakapopatikana,” taarifa ya SPA ilisema.
“Mgomo wa kususia kazi ni hatua ya kisheria na ni silaha hatari sana ambayo inaweza kusambaratisha utawala wowote duniani.”
Lengo la mgomo ni kuhakikisha serikali inashindwa kuendesha shughuli zake hali itakayoifanya baraza la jeshi kushindwa kutawala, aliongeza mwandishi wetu.
Siku ya Ijumaa , waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alizuru taifa hilo ili kuzipatanisha pande hizo mbili ambazo alikutana nazo katika mikutano miwili tofauti.
Lakini saa chache baadaye , habari zilisambaa kuhusu kukamatwa kwa Mohamed Ismat -mwanachama wa muungano wa upinzani na afisa mkuu wa benki kuu nchini Sudan.
Baadaye wanajeshi wanadaiwa kumkamata afisa mwandamizi wa SPLM-North Ismail jalab na msemaji Mubarak Ardol. Kiongozi wa chama hicho Yasir Arman pia alikamatwa siku ya Jumatano.
Habari za kuzuiliwa kwa viongozi huo zitazua kutoaminika kwa baraza la kijeshi linalotawala. Makundi ya waandamanaji yanapanga kuendelea na kampeni yao siku ya Jumapili.
Bwana Esmat na bwana Jalab ni viongozi wakuu wa muungano wa upinzani Freedom for Change , mwavuli wa upinzani unaoshirikisha viongozi wa maandamano na makundi ya waasi.
”Hii ni sawa na baraza la jeshi kusema kwamba linapinga juhudu za mpatanishi waziri mkuu wa Ethiopia ,” alisema Khalid Omar Yousef- kiongozi wa muungano wa upinzani akizungumza na shirika la habari la Reuters kufuatia kukamatwa kwa bwana Esmat.
Baraza la serikali ya mpito TMC halijatoa tamko lolote.
Muhariri wa BBC Mary Harper anasema kuwa hatua hiyo ya hivi karibuni inaonyesha kuwa upatanishi wa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed haukuchukuliwa na umuhimu mkubwa na jeshi.
Baraza hilo linaonekana limepata matumaini ya kisiasa na ufadhili kutoka kwa Saudia , UAE na Misri , mataifa ambayo hayatilii mkazo kuwepo kwa demokrasi nchini humo.
RSF, ambalo lilijulikana kama wapiganaji wa Janjaweed lilijipatia umaarufu wake baada ya kutekeleza vitendo vya kikatili katika eneo la Darfur 2003.
Wakaazi wa Khartoum wameambia BBC kwamba wanaishi kwa hofu katika mji huo.
Baadhi ya wanawake waliokamatwa na RSF waliambia BBC kwamba walipigwa na kutishia kuuawawa.
Wanasema kuwa wapiganaji hao waliwataka kunusru maisha yao na baadaye wakawafyatulia risasi.
Waathiriwa wengine wanasema walilazimishwa kunywa maji taka ambayo yalikuwa yamekojolewa.
Je mgogoro huo unaweza kutatuliwa kidiplomasia?
Siku ya Alhamisi Muungano wa Afrika ulisitisha uanachama wa Sudan mara moja na kuonya kuichukulia hatua zaidi iwapo mamlaka hayatakabidhiwa raia.
Mwenyekiti wa tume ya Muungano huo Moussa faki mahamat alitaka uchunguzi wa wazi kufanyiwa mauaji yaliotokea.
Wakati wa ziara yake mjini Khartoum , waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alizitaka pande zote mbili kuwa na ujasiri na kukubaliana kuhusu hatua zaitakazolipeleka taifa hilo katika demokrasia.
Ripoti zinasema alikuwa amependekeza kuanzisha baraza la utawala wa mpito lenye raia wanane na wanajeshi saba huku kukiwa na rais ambaye atakuwa akibadilishwa mara kwa mara. Haijulikani pendekezo hilo lilichukuliwaje.
No comments:
Post a Comment