Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, BAVICHA limeeleza kuwa linaendeleea kufuatilia kupatikana kwa dhamana ya Mwenyekiti wake Patrick Ole Sosopi ambaye alikamatwa jana akiwa mkoani Morogoro.
Kwa mujibu taarifa za awali Sosopi amekamatwa mkoani akidaiwa kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba, akiwa pamoja na aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Kwela Mkoajni Rukwa 2015, Daniel Naftal.
Akizungumza na www.eatv.tv Katibu wa BAVICHA, Julius Mwita ameeleza kuwa wanaendelea kuwasiliana na Mawakili wa chama hicho ili kuhakikisha Mwenyekiti wao anapata dhamana.
"Watu wako pale Morogoro wanaendelea kufuatilia, tumezungumza na RCO wanaendelea kumhoji lakini mpaka usiku wa jana alikuwa hajaachiwa bado", amesema Julius Mwita.
"Na tunavyoongea sasa hivi kuna wanachama wetu wengine wawili waliokwenda kusimamia uchaguzi w andani, wamekamatwa Morogoro kwenye hoteli ambayo wamefikia wameamka asubuhi wamekuta hoteli waliyofikia, imezungukwa na Askari." amesema Mwita
Mapema jana kupitia mitandao ya kijamii kulianza kusambaa kwa taarifa juu ya kukamatwa kwa Mwenyekiti huyo wa BAVICHA
www.eatv.tv imejaribu kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment