Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameahidi kutoa Tsh. Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Waziri Ummy ametoa ahadi hiyo leo wakati alipofanya ziara ya kutembelea jengo jipya la mama na mtoto (Maternity Block) katika Hospitali hiyo ili kujionea hali ya utoaji huduma kwa akina mama wajawazito na watoto.
“Ninaahidi kutoa Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la OPD ya kisasa yenye uwezo wa kupokea wagonjwa wengi zaidi tofauti na OPD iliyopo sasa”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameutaka uongozi wa Hospitali hiyo kurekebisha na kufanya maboresho katika baadhi ya maeneo yaliyoonekana kuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuyapa majina majengo yote ya Hospitali hiyo ili kuepusha usumbufu kwa wagonjwa pindi wanapotaka kupata huduma katika majengo tofauti.
No comments:
Post a Comment