Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 06 Aprili, 2019 amezindua mradi wa njia ya umeme ya msongo wa KV 220 kutoka Makambako hadi Songea na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha mabasi na barabara za lami katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Sherehe za uzinduzi wa mradi wa njia ya umeme zimefanyika katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo Unangwa Mjini Songea na zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjöberg, Mawaziri, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Godfrey Zambi.
Mradi huo umehusisha ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 245, upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako, ujenzi wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme vya Madaba na Songea na usambazaji wa umeme wa msongo wa kilovoti 33 zenye urefu wa kilometa 900 zilizounganishwa kwa wateja 22,700 katika Wilaya za Njombe, Ludewa, Mji wa Makambako, Songea Vijijini, Songea Mjini, Namtumbo na Mbinga.
Ujenzi wa mradi huo umegharimu shilingi Bilioni 216 na Milioni 941, fedha ambazo zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Sweden na Serikali ya Tanzania, na baada ya kukamilika kwake Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezima mitambo ya kuzalisha umeme kwa mafuta katika vituo 5 na hivyo kuokoa shilingi Bilioni 9.8 kwa mwaka.
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo wa kuhakikisha mradi huo unaanza kutekelezwa mara alipoingia madarakani na kwamba hivi sasa Mkoa wa Ruvuma wenye mahitaji ya megawati 12 za umeme unapata megawati 48 zitakazowezesha uanzishaji wa viwanda na vijiji vyote kupatiwa umeme ifikapo mwaka 2012.
Mhe. Kalemani amebainisha kuwa tangu Mhe. Rais Magufuli aingie madarakani idadi ya vijiji vilivyopatiwa umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijiji (REA) imeongezeka kutoka 2,018 hadi kufikia 6,464 (sawa na ongezeko la asilimia 214).
Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Andrers Sjöberg ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa uhusiano na ushirikiano mzuri na Sweden ambao umesaidia kutekelezwa kwa miradi mingi ya maji tangu miaka ya 90 na baadaye kufuatiwa na miradi ya kupeleka umeme vijijini ambako wananchi wengi wamenufaika hususani wanawake.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru nchi ya Sweden kupitia SIDA kwa ufadhili wake katika mradi huo na ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo pamoja na mradi mkubwa ambao Tanzania inaujenga hivi sasa wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji utasaidia kuinua uchumi kupitia viwanda na pia utasaidia kuokoa mazingira kwa kuwa wananchi watatumia umeme badala ya kuni na mkaa ambao unapatikana kwa kukata miti.
“Takwimu zinaonesha ekari 400,000 za miti huvunwa kila mwaka kwa lengo kupata kuni na mkaa wa kupikia, hii yote inasababishwa na umeme kidogo na wa gharama kubwa tulionao, tunapotekeleza miradi hii tutaokoa uharibifu huu wa mazingira, kwa hiyo nakuomba Mhe. Balozi ukawaeleze Mabalozi wenzako kuwa Tanzania tunapotekeleza miradi hii tunataka kuimarisha uchumi wetu na pia kuokoa misitu yetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Ametoa wito kwa Sweden na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa nishati ya umeme kupitia vyanzo mbalimbali vikiwemo gesi, makaa ya mawe, urani, upepo na joto ardhi, na pia amewataka Watanzania waongeze juhudi katika utunzaji wa mazingira.
Kabla ya kuzungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Majimaji, Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi katika eneo la Shule ya Tanga, na ujenzi wa barabara za Manispaa hiyo ambapo ameagiza miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakikana.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amesema ujenzi wa mradi huo ulioanza tarehe 25 Machi, 2018 unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba, 2019 kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.2 na utahusisha ujenzi wa kilometa 2 za barabara, eneo la kuegesha mabasi 92 na ujenzi maegesho ya magari mengine na huduma mbalimbali. Manispaa ya Songea ni miongoni mwa Halmashauri 18 zinazotekeleza mradi kama huo hapa nchini.
Majira ya jioni, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Majimaji ambapo amewahakikishia kuwa Serikali anayoiongoza inatekeleza miradi hii mikubwa ili kuimarisha ustawi wa wananchi na kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zikiwemo ujenzi wa viwanda.
“Juzi nimefungua barabara ya Mtambaswala – Mangaka – Nakapanya – Tunduru yenye urefu wa kilometa 202, jana nimefungua barabara ya Tunduru – Namtumbo yenye urefu wa kilometa 193, leo nimezindua mradi mkubwa wa umeme ambao umewaletea umeme mwingi kupita mahitaji yenu na sasa tunaanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Lumecha – Londo – Ifakara, hizi zote ni juhudi za kuimarisha fursa za uchumi, nataka mnufaike” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mawaziri wengine waliongozana na Mhe. Rais Magufuli wamewahakikishia wananchi wa Ruvuma kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za kuhakikisha wanapata pembejeo za kilimo za kutosha na kwa gharama nafuu, kuimarisha miundombinu ya barabara na ukarabati wa uwanja wa ndege.
Akiwa uwanjani Majimaji, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea ambapo ametoa shilingi Milioni 5 kwa ajili ya shule hiyo na ameiagiza TAMISEMI kuhakikisha inatatua tatizo la mabweni na vyoo.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli kesho anaendelea na ziara yake hapa Mkoani Ruvuma ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay na kuzungumza na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Songea
06 Aprili, 2019
No comments:
Post a Comment